SHIRIKA la Ugavi wa Umeme
Nchini (TANESCO) limekana kuwepo mgawo wa umeme kwa sasa huku likikiri kuwa
hali ya upatikanaji wa nishati hiyo iko katika dharura na haijarejea katika
hali ya kawaida kama inavyotakiwa.
Ufafanuzi huu unakuja baada
ya gazeti hili kuripoti hali tete ya kifedha inayolikabili shirika hili na
hivyo kutishia taifa kuingia gizani wakati wowote.
Hata hivyo TANESCO na
serikali kupitia kwa Wizara ya Nishati na Madini wamekuwa kimya kwa muda pasipo
kuzungumzia mgawo wa umeme ambao umekuwepo kwa wiki takriban mbili katika
maeneo mengi nchini.
Akizungumza jana makao makuu
ya shirika hilo Ubungo, jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Felchesmi
Mramba, alisema kuwa hakuna mgawo wa umeme kwa sasa na kwamba ikitokea serikali
ingetangaza.
Pamoja na kukanusha kuwepo
kwa mgawo, Mramba alisema ukweli ni kwamba bado nchi iko katika hali ya dharura
na hali ya umeme haijarejea katika hali yake ya kawaida kiasi cha kuondoka
katika hali ya dharura.
“Ushahidi wa kwamba bado
tuko katika hali ya dharura ni kwamba bado mitambo ya dharura tuliyokodi
kupambana na hali ya umeme inaendelea kuhitajika lakini pia mabwawa hayana maji
ya kutosha kukidhi mahitaji ya umeme bila kuhitaji mitambo ya matufa,” alisema.
Aliongeza kuwa vilevile
miundombinu ya gesi haiwapi gesi ya kutosha kuwasha mitambo yote ya gesi ya
megawati 501.
Mramba alibainisha kuwa
tangu Julai mwaka 2012 hadi Februari 2013, serikali imetumia jumla ya sh
bilioni 231.2 kama ruzuku kwa TANESCO kwa ajili ya kununua mafuta ya mitambo.
“TANESCO kutoka kwenye
mapato yake imetumia jumla ya sh bilioni 423.3 katika kipindi hicho kununulia
mafuta, hivyo fedha yote iliyotumika kununulia mafuta ndani ya kipindi hicho ni
sh bilioni 654.5,” alisema.
Mramba aliongeza kuwa
mitambo ya dharura inahitaji fedha nyingi kuiendesha kulinganisha na bei halisi
ya kuuza umeme huo. Akitolea mfano alisema kuwa ili kuzalisha zinahitajika
megawati 365 kwa mafuta (Dizeli-lita 1,368,00, HFO-LITA 500,000 na Jet A1-Lita
518,000 kwa siku.
Alisema kuwa jumla ya sh
bilioni 5.4 zinahitajika kila siku au sawa na sh bilioni 162 kwa mwezi na
kwamba mapato yanayotokana na kuuza asilimia 100 ya umeme wote unaozalishwa ni
sh bilioni kwa siku sawa na takriban sh bilioni 70.2 kwa mwezi baada ya kuondoa
kodi na tozo mbalimbali.
“Hata kama TANESCO ingeamua
isilipe mishahara wala isifanye matengenezo ya mitambo, isinunue vifaa vya
kuunganishia wateja, au isiingie gharama nyingine zozote, bado ingepata hasara
ya karibu sh bilioni 90 kila mwezi,” alisema.
Mramba aliongeza kuwa kwa
sababu kuna matumizi mengine muhimu ya kiuendeshaji, TANESCO inajikuta ikipata
hasara kubwa zaidi kwa mwezi.
Kuhusu deni la Songas,
mkurugenzi huyo alikiri kuwa ni kweli kampuni hiyo inaidai TANESCO na
akasisitiza kuwa mkataba kati ya Songas na TANESCO unaruhusu hali hiyo.
Hata hivyo, kauli hiyo
inatofautiana na kauli ya Naibu Waziri wa Nishari na Madini, George
Simbachawene, aliyesema jana asubuhi kuwa wanaoshinikiza kuwa kuna deni kati ya
Songas na TANESCO ni madalali tu.
Source:Tanzania Daima online
0 comments:
Post a Comment